Monday 5 March 2018

Afrika Kusini: Shirika lataka ukweli kuhusu mauaji ya mwanafunzi Mtanzania Baraka Naferi


Wanachama wa Shirika la Africa Diaspora Forum wamefanya mandamano nchini Afrika Kusini kushinikiza serikali ya nchi hiyo na serikali ya Tanzania kubaini ukweli kuhusu kuuawa kwa mwanafunzi raia wa Tanzania mwezi jana.

Bw Baraka Leonard Naferi, mwanafunzi wa shahada ya uzamifu, alifariki baada ya kugongwa na gari la teksi nje ya bweni la chuo kikuu.

Maafisa wa shirika hilo wameandamana kwa pamoja nabaadhi ya wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Johannesburg nje ya bweni kwa jina Sophiatown ambapo mwanafunzi huyo alikuwa anaishi.

Mshukiwa alikamatwa na polisi wa Afrika Kusini lakini baadaye akaachiliwa huru kwa dhamana.

Polisi walisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka ya mauaji.

Badala yake, Mwandishi wetu Omar Mutasa aliyeko Johannesburg anasema polisi walimfungulia mashtaka ya kuendesha gari bila leseni.

Waandamanaji wameweka shada la maua kwenye uzio wa bweni la Sophiatown alipouawa Bw Baraka.

Bw Baraka aliuawa mnamo 23 Februari.

Baadhi ya wanafunzi wanasema kuna kanda ya video za usalama ambayo inamuonesha mwanafunzi huyo akikimbia na mwanafunzi mwingine, nyuma wakiandamwa na watu wawili waliokuwa ndani ya gari la teksi.

Gari hilo linaonekana kuwakimbiza na hatimaye Baraka anagongwa mara kadha akiwa kwenye uzio wa bweni.

0 comments:

Post a Comment