Sydney,Australia.
WAKATI idadi kubwa ya Watanzania wakiwa bado hawajaketi vitini kupata chakula chao cha mchana (lunch),mabingwa wa kombe la FA nchini England,Arsenal watashuka kwenye dimba la Allianz mishale ya saa 12:30 za mchana huko Sydney,Australia kupepetana na mabingwa wa nchi hiyo,Sydney FC kwenye mchezo wao wa kwanza wa kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu England.
Arsenal ambayo iko Sydney tangu Jumatatu imeripotiwa kuwa itashusha kikosi chake kamili kuikabili Sydney FC akiwemo mchezaji wake ghali zaidi,Alexandre Lacazette iliyemnunua kutoka Lyon kwa Pauni 52 Milioni.
Mbali ya Lacazetti pia Arsenal itamtumia beki wake mpya wa kushoto,Sead Kolasinac iliyemnasa bure kutoka Schalke 04 ya Ujerumani.Aidha katika mchezo huo Arsenal itamkosa staa wake, Alexis Sanchez aliyeko mapumzikoni.
Kwa upande wao Sydney FC, watakuwa na kikosi chao chote kilichowapa ubingwa wa A-League msimu uliopita akiwemo mshambuliaji wao hatari raia wa Brazil,Bobo aliyefunga mabao 15 msimu uliopita pamoja na nahodha wao Alex Brosque aliyefunga mabao 11.
Arsenal itarejea tena dimbani kesho kutwa Jumamosi kucheza na Western Sydney FC katika mchezo wake wa pili wa maandalizi na wa mwisho nchini kabla ya kukwea pipa kuelekea nchini China ambapo itaendelea na maandalizi yake ikiwemo kucheza michezo ya kirafiki.
0 comments:
Post a Comment