Sunday, 18 June 2017

Utegemezi usio na mwamana wa serikali ya Doha kwa Marekani, kosa kubwa la Qatar



Katika hali ambayo kwenye mgogoro wa Saudia na Qatar, serikali ya Marekani imesimama upande wa watawala wa Aal Saud, Ijumaa ya juzi ya tarehe 16 Juni, jeshi la majini la Qatar lilifanya maneva ya pamoja ya kijeshi na kikosi cha baharini cha Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi.

Wizara ya Ulinzi ya Qatar sambamba na kutoa ripoti hiyo, ilitangaza kwamba, luteka hiyo ya pamoja ya baharini imezishirikisha timu 12 za vikosi vya baharini vya Marekani na Qatar. Aidha katika maneva hayo ya siku moja askari wa pande mbili walilenga shabaha na kushambulia maeneo ya adui bandia kwa kutumia mizinga na zana tofauti za baharini.


Moja ya meli za kivita za Qatar

Katika hali ambayo kwenye mgogoro wa Saudia na Qatar serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imesimama bega kwa bega na upande wa Riyadh, hapa panaibuka swali kwamba, ni nini malengo ya serikali ya Doha katika kufanya maneva ya pamoja ya kijeshi na vikosi vya baharini vya Marekani? Inaonekana kuwa, lengo kuu la Qatar la kufanya luteka hiyo ni kuendelea kufungamana kiusalama na Marekani. Hii ni kusema kuwa hadi sasa kambi ya kikosi cha anga ya Al Udeid nchini Qatar, ni kambi kubwa kabisa ya anga ya Marekani nje ya nchi hiyo ambapo jumla ya askari wake elfu 10 wa Kimarekani wapo katika eneo hilo. Wakati huo huo, kambi ya kijeshi ya Al Sailiya nchini Qatar inatumiwa kama ghala la ziada la kuhifadhia zana za kijeshi za Marekani za kuweza kutumika wakati wowote Washington itakapoingia katika vita na nchi yoyote ya eneo.


Wakati wa kujiri maneva hayo

Ukweli ni kwamba, kitendo cha serikali ya Doha cha kuzipatia Marekani kambi zake za kijeshi, ni aina fulani ya kununua usalama wake kutoka kwa Washington. Amma nukta muhimu ni hii kwamba, tunapozingatia radiamali ya serikali ya Trump katika mgogoro wa Qatar na Saudia na muundo wa kukabidhiana madaraka kutoka kwa Sheikh Hamad bin Khalifa kwenda kwa mwanawe Sheikh Tamim mwaka 2013 jambo ambalo kwa namna fulani lilifanyika kwa makubaliano ya siri baina ya Riyadh na Washington kunathibitisha kwamba, utegemezi wa Qatar kwa Marekani hauwezi kudhamini usalama wa utawala wa Aal-Thani nchini Qatar. Kwa ajili hiyo, kufanya mazoezi ya kijeshi na ununuzi wa silaha za Marekani ulioigharimu Qatar dola bilioni 12, ni mwendelezo ule ule wa makosa ya Qatar katika kuitegemea Marekani kama njia ya kununua usalama wake. Nukta ya pili ni kwamba, katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Qatar imeelezwa kwamba katika luteka hiyo ya kijeshi kati ya askari wake na Marekani, kulitumika mizinga katika kushambulia maeneo bandia ya adui. Hata hivyo swali la msingi ni kwamba, je, adui huyo bandia ni Saudia au la? Ikiwa ni Saudia, basi kwa mara nyingine tena serikali ya Doha itakuwa inafuata mwendo usio sahihi katika kuishirikisha Marekani kwenye kulinda usalama wake.


Sehemu ya kikosi cha baharini cha Qatar

Hii ni kusema kuwa, kwa mtazamo wa Washington, kama ambavyo utawala wa Kizayuni wa Israel ulivyo na nafasi kubwa kwa Marekani kuliko Saudi Arabia, ndivyo ambavyo Riyadh nayo ilivyo na nafasi kubwa kwake kuliko Qatar. Kwa mantiki hiyo, hatua ya kufanya luteka ya pamoja na katika mazingira ya hivi sasa ambapo mgogoro baina ya Qatar na Saudia pamoja na washirika wake umeshika kasi zaidi, inaonyesha kwamba, watawala wa Qatar, wana wasiwasi na matokeo ya mgogoro huo. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, sambamba na hatua za serikali ya Donald Trump wa Marekani kutokuwa na mwamana, kutokana na kuchochea kwake migogoro baina ya nchi za Kiarabu hususan kati ya Saudia na Qatar, hivi sasa Marekani ndiyo inayofaidi kwa kiasi kikubwa kiuchumi kutokana na wasiwasi wa watawala wa Qatar.


Kambi ya kikosi cha anga ya Al Udeid ya Qatar inayotumiwa na Marekani

Ukweli ni kwamba, aliyesababisha mgogoro kati ya Saudia na Qatar, ni serikali ya Marekani na hadi sasa Washington imefaidika kwa kiwango kikubwa na hali hiyo. Amma jambo moja liko wazi nalo ni kwamba, wasi wasi wa watawala wa Qatar kamwe hauwezi kuondoka kwa nchi hiyo kuendelea kufungamana na Marekani.


0 comments:

Post a Comment