Sunday, 18 June 2017

UNHCR yaipongeza Iran kwa huduma zake kwa wakimbizi



Mkuu wa ofisi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran amesifu huduma zinazotolewa na serikali ya Tehrah kwa wakimbizi.

Mulugata Zewdi Mamov amesema kuwa, huduma zinazotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wakibizi zikiwemo huduma za bima ya matibabu, kuheshimiwa haki zao za kijamii na haki ya kusoma hazitolewi katika sehemu yoyote ile duniani.

Mkuu wa ofisi ya Mfuko wa Kuhudumia Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa UNHCR mjini Mashhad amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo leo na Ali  Asghar Tahmasebi mmoja wa viongozi wa mkoa wa Golestan kaskazini mwa Iran na kubainisha kwamba, huduma na ukarimu wa Iran kwa raia wa kigeni ambao ni wakimbizi hauna mfano.


Wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran


Mwakilishi huyo wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR katika mji wa Mashhad ameeleza kuwa, Umoja wa Mataifa unaunga mkono na kuzisaidia nchi kama Iran ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa wakimbizi wa nchi mbalimbali wanaoishi hapa nchini. 

Kwa upande wake Ali Asghar Tahmasebi ambaye ni Naibu Mkuu wa mkoa wa Golestan amesema katika mazungumzo yake na mwakilishi huyo wa UNHCR kwamba, Iran imekuwa ikiwasaidia na kuwapatia huduma mbalimbali wakimbizi kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu ambayo haibaguwi baina ya raia wa nchi na nchi katika suala la kuwahudumia watu.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, Iran ina wakimbizi wapatao milioni 2 na nusu wengi wao wakiwa ni kutoka Afghanistan.

0 comments:

Post a Comment