Monday, 26 June 2017

Jukwaa la Wanawake Bunda kujadili fursa lazinduliwa


HALMASHAURI ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, imezindua Jukwaa la Wanawake ambalo malengo yake makuu ni pamoja na kuwakutanisha wanawake wote wa halmashauri hiyo ili kujadili fursa, changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi na za kimaendeleo kwa ujumla.

Jukwaa hilo limezinduliwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, ambapo zaidi ya wanawake 360 kutoka katika maeneo mbalimbali katika halimashauri ya mji wa Bunda, wameshiriki na kupeana mikakati mbalimbali ya kujiinua kiuchumi.

Akizindua jukwaa hilo, Bupilipili aliwataka wanawake wilayani hapa kujitambua na kuwa chachu ya maendeleo, kwa maana wao ni watu muhimu sana katika familia zao na jamii kwa ujumla. Aidha, aliwataka wanawake walioolewa kuacha tabia ya kuwa wategemezi na badala yake, wafanye kazi ya ujasiriamali, ili wasaidiane na waume wao kuinua uchumi wa familia zao.

Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Janeth Mayanja, alisema kuwa wanawake wamekuwa hawapati fursa za kutosha hapa nchini na duniani kote kutokana na kutokuwa na usawa katika fursa, uwezo wa kupata mitaji na ajira.

Mratibu wa jukwaa hilo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, Stella Kazinja, alisema kuwa kupitia jukwaa hilo, wanawake wataongeza uelewa katika masuala ya uchumi, biashara, upatikanaji wa mitaji, sheria za nchi katika masuala ya uchumi na jinsi ya kujitegemea kiuchumi.79

0 comments:

Post a Comment