Sunday, 29 October 2017

Ni Wakenya Rock City Marathon 2017

Abrahamu Too kutoka Kenya ameibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za km 42 Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza leo baada ya kumaliza kwa muda wa saa 02:22:45, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo Moris Motima aliyetumia muda wa saa 02:23:19.

Kivutio katika mbio hizo ilikuwa ni Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Bi Juliana Shonza ambae mbali na kuzindua mbio hizo pia alishiriki katika mbio za km 3 akiambatana na viongozi wengine wa serikali.

Nafasi ya tatu katika mbio hizo pia ilichukuliwa Mkenya George Onyacha aliyetumia muda wa saa 02:23:27, ikiwa sekunde chache nyuma ya mpinzani wake.

Katika mbio hizo zilizoanzia na kuhitimishwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo ilishuhudiwa nafasi ya kwanza hadi ya saba zikishikwa na wakimbiaji kutoka nchini Kenya huku nafasi ya nane ikienda kwa Mtanzania Paschal Mombo alietumia muda wa saa 02:30:43.

Akizungumzia siri ya ushindi wake, mbali na kusifia uratibu mzuri wa mbio hizo uliomuwezesha kukimbia bila changamoto yoyote Too alisema ni kujituma kufanya zaidi mazoezi na kukaa kambini muda mrefu ili kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu.

“Maandalizi ya mwaka huu ni mazuri na washiriki wameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka jambo linalotufanya wanariadha kujiwekea mikakati mizuri ili kuweza kukabiliana na ushindani mkali uliopo katika mbio hizi na ninashukuru Mungu nimefanikiwa,” amesema.

Upande wa wanawake mshindi wa kwanza ni Mkenya Alice Gradys Otero aliyetumia muda wa saa 02:48:18 akifuatiwa na Mkenya mwenzie Tecla Chebet  aliyetumia saa 02:54:28 huku nafasi ya tatu ikishikwa na Mkenya Flavious Kwamboka alietumia muda wa saa 02:57:32.

Mtanzania Brabuelia Bryton kutoka mkoani Moshi alishika nafasi ya sita kwa upande wa wanawake katika mbio hizo akitumia saa 03:14:41.

Washindi wa kwanza katika mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya nane jijini humo  waliibuka na kitita cha Sh 4 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh 2 mil na washindi watatu Sh 1,000,000 mil.

Kwa upande wa mbio za km 21 Peter Limo kutoka Kenya aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:05:24, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo George Wayaki aliyetumia muda wa saa 01:05:50.

Nafasi ya tatu katika mbio hizo pia ilichukuliwa Mtanzania Chacha Boy aliyetumia muda wa saa 01:05:59, ikiwa sekunde tisa tu nyuma ya mpinzani wake.

Upande wa wanawake mshindi wa kwanza ni Mkenya Dorifin Omare aliyetumia muda wa saa 01:17:12 akifuatiwa na Mkenya mwenzie Alice Mogiare aliyetumia saa 01:18:30 huku nafasi ya tatu ikishikwa na Mkenya Maiselina Issa alietumia muda wa saa 01:19:55.

Mtanzania Siatha Romanus kutoka mkoani Arusha alishika nafasi ya sita kwa upande wa wanawake katika mbio hizo akitumia saa 01:25:58.

Katika mashindano hayo ilishuhudiwa washiriki ambao pia ni wadhamini wa mbio hizo kutoka  makampuni ya PUMA, Tiper, NSSF, RedBull,  Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), New Mwanza Hotel, EF Out door, CF Hospital, KK Security, na kampuni ya uchapishaji ya SDS wakishiriki kikamilifu katika mbio za KM 5 sambamba na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Naibu Waziri Shonza alisema aliwapongeza washiriki na waandaaji wa mbio hizo na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja ili kurejesha hadhi ya mchezo wa riadha nchini.


Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Bi Juliana Shonza (wa pili kulia) akishiriki katika mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza leo ambapo alikimbia mbio za km 3 akiambatana na viongozi wengine wa serikali.

“Tanzania inaweza kurejea katika ramani ya dunia kwenye michezo kama tukijikita katika maandalizi mazuri ya kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu nchini hasa kuanzia ngazi ya shule za msingi,” amesema.

Naye Rais wa Shirikisho la riadha nchini (RT) ambae pia ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu Bw Anthony Mtaka mbali  mbali na kuwapongeza waandaaji wa mbio hizo alisema licha ya wingi wa washiriki kutoka ndani ya nchi bado taifa linakabiliwa na uhaba wa wanaridha wa mbio ndefu yaani km 42 na wachache wanaofanya vizuri kwenye mbio hizo wamekuwa wakishindwa kushiriki mbio kama hizo zinazofanyika ndani ya nchi.

0 comments:

Post a Comment