Saturday, 5 August 2017

Jela miaka 120 kwa unyang’anyi


WATU wawili wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 120 jela baada ya kuopatikana na hatia ya makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Waliohukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara ni Nyatali Mashine au Masiaga Chacha (35) na Samson Chacha marufu kama Mwita Pius Kipepeo (30), wote wakazi Tarime mkoani Mara.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Karim Mushi, alisema anawatia hatiani kutumikia kifungo hicho, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila kuacha shaka yoyote.

Awali, mwendesha mashitaka Jonas Kaijage, aliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja, walitenda makosa hayo ya unyang’anyi wa kutumia silaha Novemba 23, 2015 majira ya saa saba usiku, katika mtaa wa Mapinduzi mjini Bunda, nyumbani kwa Dionisia Prosper.

Kaijage alidai kuwa watu hao waliokuwa na silaha mbalimbali ikiwemo bunduki aina ya SMG, walivamia nyumbani hapo na kuiba Sh. milioni 1.7 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Alidai kuwa baada ya kufanya ujambazi huo, watu hao walifyatua risasi kadhaa hewani kwa ajili ya kutishia wananchi na kwamba walipita mtaa wa Genge la Jioni na kumuua kwa kumpiga risasi kijana mmoja aliyekuwa anauza vitumbua baada ya kuwatambua.

Aliendelea kudai kuwa baadaye mshitakiwa wa kwanza, Chacha alikamatwa wilayani Tarime mpakani Sirari na kupekuliwa kwake katika mtaa wa Majengo wilayani Bunda na kukutwa na bunduki hiyo pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na shoka moja, vitu ambavyo alikuwa amevificha uvunguni mwa kitanda chake.

Kaijage alidai kuwa baada ya kuhojiwa na polisi alimtaja mwenzake huyo ambaye ni mshitakiwa wa pili, aliyekamatiwa katika nchi jirani ya Kenya.

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Kaijage aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washitakiwa kwa madai kuwa ni majambazi wazoefu na kwa vipindi tofauti waliutikisa mji wa Bunda kwa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.

Kaijage alidai kuwa washtakiwa hao, kulingana na umri wao, walipaswa kufanya kazi halali za kujipatia kipato maana wanazo nguvu za kutosha na si kufanya uharifu ukiwamo ujambazi wa kutumia silaha.

Aidha, washtakiwa hao waliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu, ombi ambalo lilitupiliwa mbali na Hakimu Mushi, aliyesema ameitafsiri sheria baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa mahakamani pasipo kuacha shaka yoyote na upande wa mashtakia kwamba ni kweli walitenda makosa hayo.

Alisema kuwa kwa jinsi hiyo kila mshitakiwa anahukumiwa kifungo cha miaka 60 jela kwa maana kila kosa atatumikia kifungo cha miaka 30.

Hata hivyo, alisema kwa vile adhabu zote zinakwenda pamoja, kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela, ili kuwa fundisho kwake na kwa watu wengine wenye nia au tabia ya kufanya uharifu.
00000

0 comments:

Post a Comment