Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano inawataka watumishi wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kuheshimiana na atakayeshindwa kufanya hivyo hatavumiliwa. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Julai 20, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Songwe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Songwe.
Amesema watumishi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi yaweze kufikiwa. Pia waheshimiane sehemu za kazi na kila mtu azingatie mipaka ya madaraka yake.
"Mkurugenzi hapa hamsikilizi Mkuu wa wilaya anaondoka kituo cha kazi bila ya kuaga na amewagawa wakuu wa Idara. Namtaka afanye mabadiliko ya utendaji wake ndani ya miezi miwili na Mkuu wa Mkoa fuatilia jambo hili."
Waziri Mkuu pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote wasimamie utendaji wa wakurugenzi wa Halmashauri kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo.
"Serikali hii si ya mchezo. Serikali hii inahitaji watumishi waadilifu wa kuwatumikia Watanzania." alisisitiza Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameanza leo ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Songwe
0 comments:
Post a Comment