Monday, 10 July 2017

RC GODFREY ZAMBI awasimamisha kazi watumishi sita wa vitengo mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi.


Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bwana  GODFREY ZAMBI amewasimamisha kazi watumishi sita wa vitengo mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi ili  kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi kutokana na utendaji wao usioridhisha.

Akizungumza na Madiwani wa Halmashauri hiyo Zambi amewataja waliosimamishwa kuwa ni Wakuu wa Idara za Sheria inayoongozwa na NYAMANDE KASIMIR,Mkaguzi wa Ndani, Bwana  IDD MBOWETO, Mtunza Hazina, Bwana  GERVAS NGOMANO, Kaimu Mhandisi wa Ujenzi Bwana ASWILE MWASAGA, Bwana HAROUN KINAWA wa Ushirika pamoja na Bwana  DANIEL KASEMBE ambaye anakaimu kitengo cha Ugavi katika Halmashauri hiyo.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa wafayakazi hao wameshindwa kuzijibu hoja 36 ambazo zimebainika na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali- CAG, zikiwemo kutofuatilia madai ya muda mrefu ya Shilingi Milioni 669 na Laki- 6, kutosimamia makusanyo ya mapato ya madeni kutoka AMCOS mbalimbali yanayofikia Shilingi Milioni 127 na Laki- 8 na kufanya mikataba bila kuzingatia taratibu.

Kutokana na hali hiyo Bwana ZAMBI amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bwana  RAMADHAN KASWA kuunda tume ya kuchunguza tuhuma za watumishi hao na watakaobainika kuwa na makosa hatua za nidhamu zitachukuliwa dhidi yao.

0 comments:

Post a Comment