Wednesday 14 June 2017

Saif al-Islam: ICC yataka mwana wa Gaddafi akamatwe


Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) imeitaka serikali ya Libya kumkamata na kumsalimisha Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo marehemu Kanali Muammar Gaddafi.

Saif aliachiliwa huru na kundi la wanamgambo wiki iliyopita baada ya kuzuiliwa kwa miaka sita.

Amekuwa akisakwa na mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague, Uholanzi kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu ambao anadaiwa kuyatekeleza wakati wa maasi yaliyopelekea kuondolewa madarakani kwa babake mwaka 2011.

Bado haijabainika yuko wapi kwa sasa.

    Mwana wa Gaddafi aachiliwa huru Libya
    Je mwana wa Gaddafi anaweza kuiongoza Libya?

Serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imeshutumu kuachiliwa huru kwake.

Inahofiwa kwamba huenda kuwa huru kwake kukachangia kuyumbisha uthabiti wa taifa hilo kisiasa na kiusalama.

Taarifa nchini Libya zilidokeza kwamba huenda yupo mashariki mwa Libya, kwa jamaa zake.

Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou Bensouda amesema afisi yake bado inajaribu kuthibitisha taarifa kuhusu kuachiliwa kwake, na ameitaka serikali ya Libya na mataifa mengine kumkamata na kumsalimisha wka mahakama hiyo.

"Libya ina wajibu wa kumkamata na kumsalimisha mara moja Bw Gaddafi kwa ICC, bila kujali kama kuna sheria inayodaiwa kutumiwa kumpa msamaha Libya," amesema kupitia taarifa.

Wanamgambo wa Abu Bakr al-Siddiq Battalion wanadaiwa kumuachilia huru baada ya ombi kutoka kwa "serikali ya muda".

Serikali hiyo - yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo - ilikuwa tayari imetoa msamaha kwa Saif al-Islam.

Hata hivyo, alikuwa amehukumiwa kifo na mahakama mjini Tripoli, magharibi mwa nchi hiyo bila yeye kuwepo mahakamani.

Maeneo ya magharibi yanatawaliwa na serikali inayopingana na serikali ya mashariki mwa Libya, lakini serikali hiyo ya magharibi yenye makao yake makuu Tripoli ndiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kwa kirefu, inafahamika kama Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Taarifa zilizowahi kutolewa awali kuhusu kuachiliwa kwa Saif al-Islam Gaddafi baadaye zilibainika kuwa na uongo.

Saif al-Islam, alikamatwa Novemba 2011 baada ya kuwa mafichoni kwa miezi mitatu kufuatia kuondolewa madarakani kwa babake, Kanali Gaddafi.

Awali, alikuwa ametekeleza mchango muhimu katika kufufua na kujenga upya uhusiano kati ya serikali ya babake na nchi za Magharibi baada ya 2000.

Alitazamwa na mataifa hayo kama mwanamageuzi na mpenda mabadiliko katika serikali ya babake.

Lakini baada ya maasi ya mwaka 2011, alijipata akituhumiwa kuchochea ghasia na mauaji ya waandamanaji.

Miaka minne baadaye, alihukumiwa kuuawa kwa kupigwa risasi baada ya kukamilishwa kwa kesi iliyomhusisha yeye na washirika 30 wa karibu sana wa Gaddafi.

Saif al-Islam: Mrithi aliyegeuka mfungwa

    Juni 1972: Azaliwa Tripoli, Libya, mwana wa pili wa kiume wa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi
    Februari 2011: Maasi dhdii ya utawala wa Gaddafi ryaanza
    Juni 2011: Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) yatoa kibali cha kukamatwa kwa Saif al-Islam kwa tuhuma za kutenda makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu
    Agosti 2011: Aukimbia mji mkuu baada ya Tripoli kutekwa an wapiganaji waliokuwa wanaipinga serikali; atorokea Bani Walid
    Oktoba 2011: Babake na kakake mdogo wauawa
    19 Novemba 2011: Akamatwa na wanamgambo akitorokea Niger, kusini mwa Libya. Azuiliwa Zintan
    Julai 2015: Ahukumiwa kifo na mahakama Tripoli bila yeye kuwepo mahakamani
    Juni 2017: Aachiliwa huru baada ya msamaha uliotolewa na moja ya serikali mbili zinazoshindania kuongoza Libya

Gaddafi: Kumuomboleza 'masihi wa Afrika'

0 comments:

Post a Comment