Katika hatua inayohesabiwa kuwa ni uingiliaji wa serikali mpya ya Marekani dhidi ya Venezuela, Rais Donald Trump wa nchi hiyo amekutana na mke wa Leopoldo López, kiongozi mkuu wa upinzani anayezuiliwa katika jela nchini Venezuela.
Katika kikao hicho, Trump amemtaka Rais Nicolás Maduro wa Venezuela kumuachilia huru mwanasiasa huyo pamoja na wapinzani wengine ambao wamefungwa jela kutokana na harakati zao dhidi ya serikali ya Caracas. Kwa hakika hatua ya Rais Trump ni ujumbe kwa serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela kuhusiana na kuendelezwa siasa za huko nyuma za Washington dhidi ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta ya Amerika ya Latini.

Kama kawaida hatua ya rais huyo mpya wa Marekani, imewakasirisha mno viongozi wa Caracas. Ukweli ni kwamba viongozi wa Venezuela si tu kwamba hawashuhudii mabadiliko yoyote katika siasa za kiuadui za hapo kabla za Marekani dhidi ya nchi yao, bali inaonekana kwamba serikali ya Rais Donald Trump itatekeleza siasa za kimpangilio na kali zaidi dhidi ya Caracas. Suala hilo ndilo limemfanya Rais Nicolás Maduro wa Venezuela kutoa indhari kali kwa Trump juu ya kufeli siasa zake hizo kama ilivyokuwa katika kipindi cha Obama na mtangulizi wake, yaani George W. Bush. Wakati huo huo, Rais Maduro ameendelea kuonyesha nafasi chanya ya nchi yake katika eneo la Amerika ya Latini na eneo la Caribbean kwa ujumla, sanjari na kusisitizia kuendelea serikali ya mrengo wa kushoto nchini Venezuela katika kupambana na njama za Washington.

Hadi sasa siasa za Marekani dhidi ya Venezuela ni zenye ncha mbili za ndani na nje. Kwa upande wa ndani siasa hizo zimejengeka juu ya kuunga mkono wazi wazi upande wa upinzani kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kushoto ya Caracas. Katika fremu hiyo Marekani inaunga mkono mapendekezo ya wapinzani hususan njama za kuitishwa kura ya maoni kwa lengo la kumuondoa madarakani Rais Maduro. Ama upande wa nje pia Washington inaendeleza vikwazo vyake dhidi ya Venezuela kwa ajili ya kuidhoofisha serikali na hivyo kujaribu kuongeza kiwango cha kutoridhishwa raia wa nchi hiyo na serikali.

Huko nyuma na kupitia vikwazo kwa ajili ya kushadidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Caracas, mwezi Machi mwaka 2015 rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alitoa amri ya utekelezaji ambapo aliitaja Venezuela kuwa tishio kwa uslama wa taifa la Marekani. Kwa mujibu wa amri hiyo, baadhi ya viongozi wa Venezuela waliwekewa vikwazo. Aidha katikati ya mwezi Januari mwaka 2016 Obama alitia saini dikrii ya kuendelezwa vikwazo hivyo hadi tarehe 13 Januari mwaka 2018. Kwa mtazamo wa Washington, uungaji mkono kwa upinzani na kadhalika vikwazo dhidi ya Venezuela, hatimaye vitaweza kuisambaratisha serikali ya Rais Nicolás Maduro.

Tangu ilipoingia madarakani serikali ya mrengo wa kushotoya Venezuela, yaani tangu alipoingia madarakani Hugo Chávez, rais wa zamani wa nchi hiyo, Marekani imekuwa ikitekeleza siasa hasi na za uhasama dhidi ya viongoi wa nchi hiyo. Katika fremu hiyo serikali ya Caracas kwa mara kadhaa imekuwa ikilalamikia hatua za uingiliaji za Marekani huku ikiwasilisha mashtaka yake kwa asasi za kieneo na kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo. Mienendo ya Marekani katika kipindi cha miaka 18 iliyopita, inaonyesha kwamba, Washington haijaridhishwa hata kidogo na kuingia madarakani serikali ya mrengo wa kushoto huko Venezuela na kulichukuliwa suala hilo kuwa linalopingana na maslahi yake katika eneo zima la Amerika ya Latini. Kwa kuzingatia ushahidi uliopo, tunaweza kutabiri kuwa, hivi sasa Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni wa mrengo wa kulia, si tu kwamba hafurahishwi na kuendelea kusalia madarakani serikali ya sasa ya Caracas, bali ataendeleza njama chafu kwa ajili ya kuidhoofisha zaidi serikali hiyo kwa shabaha ya kuiondoa madarakani.
0 comments:
Post a Comment