Monday, 27 February 2017

Sherehe za tuzo za Oscar dhidi ya Rais Donald Trump

Sherehe za 89 za tuzo za Academia ya filamu ya Oscar zimefanyika, ambapo filamu ya Forushande (The Salesman) iliyotengenezwa na mtengenezaji filamu wa Kiirani Asghar Farhadi imeibuka mshindi katika kitengo cha filamu za kigeni kwenye Akademia ya Filamu ya Marekani.
Hii ni mara ya pili kwa Asghar Farhadi kunyakua tuzo ya Oscar katika kitengo cha filamu  za kigeni. Ukiachilia mbali upande wa kitaalamu na kiufundi wa filamu ya Forushande (The Salesman) ambao umewavutia waamuzi wa Tamasha la Filamu la Oscar, kupatiwa tuzo filamu hiyo ya Kiirani ni ujumbe wa wazi dhidi ya sera zilizo dhidi ya wahajiri za serikali mpya ya Marekani. Hatua ya Oscar ya kumpatia tuzo mtengeneza filamu wa Kiirani ni upinzani wa wazi dhidi ya amri iliyozusha makelele mengi ya Donald Trump ya kuwapiga marufuku raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini Marekani.
Kufuatia kutangazwa kwa amri hiyo, Asghar Farhadi na wachezaji wote katika filamu ya The Salesman walitangaza kutoshiriki katika hafla ya tuzo za filamu ya Oscar huko Marekani wakilalamika na kuonesha upinzani wao dhidi ya amri ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump inayowapiga marufuku raia wa nchi za Waislamu kuingia Marekani.
Asghar Farhadi, mtengenezaji filamu wa Kiirani
Asghar Farhadi aliwakilishwa katika hafla hiyo na Anushe Ansari mwanamke wa kwanza Muirani kusafiri anga za mbali na Firouz Naderi Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Marekani la Utafiti wa Anga (NASA) ambaye pia ni Muirani. Baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Asghar Farhadi, Bi Anousheh Ansari alisoma ujumbe uliokosoa siasa za kufarakanisha watu na zilizo dhidi ya wahajiri za serikali ya Trump. Hotuba yake hiyo fupi ilishangiliwa mno na hadhirina walioiwakilisha jamii ya kiutamaduni ya Marekani.
Hata kama daima tuzo za filamu za Oscar zimekuwa na utashi wa kisiasa, lakini sherehe za Oscar mwaka huu zimedhihirisha juu ya kuweko pengo kubwa la kiadiolojia nchini Marekani na makabiliano baina ya sekta ya utangenezaji filamu nchini humo na ikulu ya White House. Harakati ya kiliberali nchini Marekani ambayo ina satua na ushawishi mkubwa katika Sekta ya Filamu ya Hollywood ina wasiwasi mkubwa na mipango ya uhafidhina ya serikali ya Trump. Mipango kama ya kupiga marufuku uhajiri kwa misingi ya utaifa na udini, kujengwa ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na kuvikandamiza vyombo vya habari vinavyoikosoa serikali ya Trump, ni miongoni mwa mambo ambayo yamezusha hatari ya kukua harakati za kufurutu ada nchini Marekani zinazoshabihiana na Ufashisti.
Filamu ya Forushande (The Salesman) iliyopata tuzo ya Oscar mwaka huu
Kwa msingi huo, sherehe za utoaji tuzo za Oscar zinazohesabiwa kuwa moja ya matukio muhimu mno katika sekta ya filamu ulimwenguni zimegeuka na kuwa changamoto kubwa kwa siasa za serikali ya Trump. Kwa mfano, waamuzi wa Oscar wameipatia tuzo filamu ya Kiirani ya Forushande, mtengenezaji filamu aliyeshinda tuzo ametoa taarifa ya kupinga siasa za Trump zilizo dhidi ya wahajiri na hadhirina wamempigia makofi na kupongeza hotuba iliyopinga sera za Trump. Si hayo tu, bali hata mmoja wa waendeshaji wa shughuli hiyo amefanyia mzaha ada na mazoea ya Trump kwa kutuma jumbe katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter. 
Hata nje ya mipaka ya Marekani, kupatiwa tuzo filamu ya Kiirani ya Forushande kumegeuka na kuwa pozo na kitulizo kwa hujuma zenye misimamo mikali za Trump. 
Masaa machache kabla ya kufanyika sherehe za Oscar huko Los Angeles Marekani, maelfu ya watu walikusanyika katika medani ya Trafalgar  mjini London Uingereza ili waweze kushuhuhudia bure filamu ya Forushande. Sadiq Khan Meya Mwislamu wa jiji la London mwenye asili ya Pakistan alihutubu kabla ya kuonyeshwa filamu hiyo akikosoa vikali amri ya Rais Trump ya kupiga marufuku kuingia nchini Marekani raia wa nchi saba za Kiislamu.
Shahab Hussein na Taraneh Alidoosti waliocheza katika filamu ya Forushande
Kupokewa kwa wingi filamu ya Forushande na watu wa matabaka na kaumu mbalimbali ni ishara ya wazi kwamba, uwekaji mipaka usio na misingi na kujenga kuta kwa misingi ya kaumu na dini ni jambo lisilokubalika katika kila kona ya dunia.
Hata hivyo shakhsia ya Trump na utendaji wake akiwa Rais wa Marekani vinaonyesha kwamba, hashughulishwi sana na upinzani na malalamiko hayo. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, kusimama kidete mkabala na harakati ya kilimwengu ya kupinga ubaguzi hata kwa mtu kama Trump halitakuwa jambo jepesi na sahali hata kidogo.

0 comments:

Post a Comment