Wednesday 14 June 2017

Wahamiaji 100 waokolewa jangwani Niger


 Wahamiaji wengi huvumilia hatari na changamoto nyingi kusafiri kwenda Ulaya 

Takriban wanaume 85 pamoja na wanawake wamepatikana wakiwa wachovu na wakiwa wamekosa maji mwilini katika jangwa la Sahara katika jimbo la Agadez.

Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti taarifa za baadhi yao wakisema kuwa wamekuwa wakiteswa na baadae kutelekezwa jangwani bila chakula wala maji na wafanya biashara haramu wa kuwasafirisha watu.

Wanajeshi waliokuwa wakifanya doria ndio waliowaokoa siku kadhaa zilizopita na kuwaleta katika ofisi za shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM) kaskazini mashariki mwa mji wa Dirkou, karibu na mpaka na Libya.

Kulingana na IOM, wengi wa wahamiaji hao ni kutoka katika nchi za Nigeria, Senegal na Burkina Faso.



Hivi karibuni watahamishiwa katika eneo la Agadez kabla ya kurejeshwa katika nchi zao za asili.

Maafisa katika eneo hilo wanasema idadi ya vifo vinavyotokea jangwani imeongezeka tangu serikali ilipoidhinisha sheria ya kupiga marufuku biashara haramu ya kusafirisha wahamiaji, ambapo anayepatikana na hatia hufungwa jela miaka 30.

Katika kukwepa vikosi vya usalama, wanaofanya biashara ya kuwasafirisha wahamiaji hutumia njia za mbali za jangwani ambazo hazina vyanzo vya maji. 


 Wahamiaji wanaelezwa kuwa walitelekezwa jangwani karibu na kisima.


Mwaka jana, Shirika la kimataifa lawahamiaji lilirekodi zaidi ya wahamiaji laki tatu walioelekea kaskazini mwa Niger kupitia jangwani.

Mapema mwezi huu, wanaume 44 wanawake na watoto waliokuwa wakielekea Ulaya walipatikana wakiwa wamekufa jangwani katika jimbo la Agadez.

Gari lao lilikuwa limeharibika.

Niger ni moja ya lango wanalopitia wahamiaji wakielekea barani Ulaya kupitia Libya. Eneo hilo la jangwani ndio sehemu ya hatari ya safari kwa wahamiaji.

0 comments:

Post a Comment