Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa, jeshi la serikali ya Burundi linaendelea kuteka nyara, kutesa na kuua wananchi bila ya kuchukuliwa hatua yoyote.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Septemba mwaka jana, Fatsah Ouguergouz amesema tume hiyo imekusanya ushahidi 470 kuhusu ukiukwaji wa sheria na uhalifu uliofanyika nchini Burundi tangu mwaka 2015 ambao amesema unaakisi hofu kubwa iliyoenea miongoni mwa watu waliokimbia nchi hiyo.
Fatsah Ouguergouz ameongeza kuwa, tume hiyo imeshtushwa mno na ukatili na unyama mkubwa ulioelezwa kufanyika nchini Burundi.
Mwenyekiti wa Tume na Uchunguzi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, baadhi ya wahanga wa ukatili huo ambao aghlabu yao ni vijana wanachama wa vyama vya upinzani au raia wanaotuhumiwa kuunga mkono au kuwa wanachama wa makundi yanayobeba silaha, wameeleza mateso yanayofanyika kwa mpangilio maalumu na mienendo ya kikatili ya maafisa wa Idara ya Upelelezi ya Taifa na polisi ikisaidiwa na wanamgambo wa Imbonerakure.
Balozi wa Burundi katika Umoja wa Mataifa, Rénovat Tabu amekanusha madai hayo na kusema wachunguzi wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa wamepuuza juhudi zinazofanywa na serikali ya Bujumbura za kurejesha amani na usalama nchini humo.
Zaidi ya watu 700 wameuawa na wengine wanaokadiriwa kuwa laki nne wamekimbilia katika nchi jirani tangu Rais Pierre Nkurunziza alipogombea kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo licha ya upinzani mkubwa wa vyama vya upinzani ambavyo vilisema ni kinyume cha katiba na makubaliano ya Arusha.
0 comments:
Post a Comment