Thursday 15 June 2017

Saudi Arabia, muungaji mkono wa ugaidi kifedha



Saudi Arabia ni muungaji mkono mkubwa wa kifedha wa makundi ya kigaidi kieneo na kimataifa na ushahidi na nyaraka nyingi zilizopo katika uwanja huo zinathibitisha wazi kwamba nchi hiyo inayoendeshwa kiukoo imewanunua mamluki wengi wa nchi za eneo kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya ugaidi katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.



Hayo yalisema jana Jumatano na Sayyid Mahmoud Alawi, Waziri wa Usalama wa Iran ambapo aliashiria pia kusambaratishwa kwa timu na makundi ya kigaidi katika mikoa ya Sistan Baluchestan na Kurdestan nchini hapa. Kwa miaka mingi sasa Iran imekuwa ikilengwa na ugaidi na kwa msingi huo inatambua vyema udharura wa kupambana na uovu huo sugu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo ikatenga siku maalumu katika kalenda yake ambayo ni tarehe 30 Agosti kila mwaka, kuwa Siku ya Kupambana na Ugaidi. Katika miaka ya hivi karibuni, makundi ya kigaidi yanayodhaminiwa kifedha na kisilaha na nchi za Marekani na Saudi Arabia yamekuwa yakitekeleza jinai za kutisha katika nchi za eneo zikiwemo Iraq, Syria na Afghanistan. Ugaidi uliotekelezwa wiki iliyopita na magaidi wa Daesh, katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na vilevile kwenye kaburi la Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa Mfumo wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa ambapo watu 17 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa ni sehemu ya ugaidi huo.

Maafisa usalama wakipambana na magaidi walioshambulia bunge la Iran wiki iliyopita


Kidole cha lawama kinaelekezewa utawala wa Riyadh kuhusiana na matukio hayo ya kigaidi mjini Tehran kwa kutiliana maanani uungaji mkono wa Saudia kwa vitendo kama hivyo. Siku chache zilizopita, Muhammad Salman, Waziri wa Ulinzi wa Saudia katika mohijiano na jarida la Foreign Affairs na hata bila ya kuwa na haya alisema wazi kuwa utawala wa nchi hiyo umeamua kuhamishia ugaidi na machafuko katika ardhi ya Iran. Bila shaka matamshi hayo yanathibitisha wazi ufinyu wa fikra na taasubi za kijahili za watawala wa kiukoo wa Saudi Arabia kuhusiana na Iran. Baada ya kuaga dunia Mfalme Abdallah bin Abdul Aziz, mfalme wa zamani wa Saudia, watawala wa hivi sasa wasio na uzoefu wala uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya kieneo wameamua kutekeleza siasa za uhasama dhidi ya Jamuri ya Kiislamu ya  Iran. Siasa hizo katika hatua ya kwanza zimezua mivutano mikubwa katika eneo na kisha kujaribu kuingiza ugaidi na mivutano hiyo ndani ya ardhi ya Iran. Watawala vijana wasio na uzoefu na walio na tamaa ya utawala wa Saudi Arabia wanadhani kuwa wataweza kuupatia uhai mpya utawala unaoendelea kudhoofika wa nchi hiyo katika eneo kwa kuchochea mivutano na ugaidi.

Muhammad Salman, Waziri wa Ulinzi wa Saudia akiwa na Rais Donald Trump wa Marekani


Kufikia sasa Watawala wa Aal Soud wametumia fedha nyingi kudhamini makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati. Mfano wa wazi wa hilo ni uungaji mkono wao mkubwa wa kifedha kwa makundi ya kigaidi likiwemo la Daesh, yanayofanya uharibifu na jinai za kutisha dhidi ya watu wasio na hatia huko Syria na Iraq. Watawala wa Riyadh kwa hakika wamehatarisha usalama wa eneo na wa sehemu nyingine za dunia kupitia siasa hizo za kuunga mkono makundi ya kigaidi. Siasa hizo za kuzua mivutano na kueneza ugaidi zimeongezeka sana katika siku za hivi karibuni hasa kufuatia safari ya Rais Donald Trump wa Marekani huko Riyadh. Katika hali ambayo viongozi wengi wa dunia waliomboleza na kutangaza mfungamano wao na serikali ya Tehran kutokana na ugaidi uliotekelezwa na magaidi wanaoungwa mkono na Saudia mjini Tehran, hatua ya Trump ya kuwakejeli viongozi wa Iran katika hali hiyo ya msiba kwa kudai kuwa nchi zinazounga mkono ugaidi ndizo zenyewe zinazokuwa wahanga wa vitendo vya ugaidi, iliwashangaza wengi.

Rais Trump akikaribishwa na Mfalme Salman wa Saudia


Wajuzi wa mambo wanasema kuwa matamshi hayo yasiyo na ukweli wowote ya Trump yalitolewa kwa ajili ya kujaribu kuitenga Iran katika eneo na hatimaye kuilazimisha ilegeze misimamo yake kuhusiana na masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa, suala ambalo wanasema halitafanikiwa bali hata huenda likavuruga uhusiano wa Ulaya na Marekani yenyewe. Bila shaka siasa hizo za Marekani na Saudia za kuunga mkono makundi ya kigaidi dhidi ya Iran zimeshawahi kushuhudiwa tena huko nyumba ambapo nchi hizo zimekuwa zikiunga mkono kwa miaka mingi kundi la kigaidi la Munafiqeen dhidi ya mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Kwa kuzingatia hali hiyo uungaji mkono wa Saudia kwa ugaidi kwa ushirikiano wa Marekani kwa ajili ya kuvuruga uthabiti wa Iran sio tuhuma bali ni ukweli unaothibitishwa kwa nyaraka na uzoefu wa huko nyuma ambapo watawala wa Riyadh na Washington wamekuwa wakichukua misimamo ya uhasama dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu. Suala hilo linathibitisha wazi kwamba jambo lililo na umuhimu kwa watawala hao ni kufikia malengo yao hata kama hilo litakuwa na maana ya kutumiwa moja kwa moja makundi ya kigaidi. Ukweli wanaousahau ni kwamba ugaidi ni tishio kwa usalama wa kila mtu na hata kwa waungaji mkono hao wenyewe wa ugaidi.

0 comments:

Post a Comment