Saturday 17 June 2017

WAUGUZI SINGIDA WATIWA MBARONI KWA TUHUMA YA UZEMBE WAKIWA KAZINI

Jeshi la Polisi mkoa wa Singida linawashilia wauguzi  Salma Rashidi Mkoko (51) na Spesioza (40) waajiriwa wa hospitali ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida, kwa tuhuma ya uzembe wakiwa kazini.
Wauguzi hao kwa pamoja, wanatuhumiwa kushindwa kumwondolea mpira mtoto Sesilia Dastan mwenye umri wa miaka minne waliyomfunga mkononi na kusababisha mkono kuvimba.
Mtoto huyo alikaa na mpira  kwenye wodi ya watoto hospitali ya wilaya ya Manyoni kwa saa nane, huku ikiwa imembana.
Imeelezwa kwamba juni sita mwaka huu majira ya asubuhi wauguzi hao,walimfunga mkono mtoto Sesilia mkazi wa kijiji cha Sasilo wilaya ya Manyoni.Lengo lilikuwa ni kutafuta mishipa ili waweze kumwekea dripu. Hata hivyo hawakuweza kupata mishipa kwenye mkono.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP. Bebora Magiligimba, alisema tukio hilo lilitokea Juni, 7 mwaka huu mchana, daktari wa zamu wakati akikagua wagonjwa, alibaini mpira ukiwa umesahaulika kwenye mkono wa mtoto Sesilia.


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP. Debora Daud Magiligimba, akitoa taarifa juu ya kukamatwa kwa wauguzi hospitali ya wilaya ya Manyoni kwa tuhuma ya uzembe wakati kazini. (Picha na Nathaniel Limu)

“Daktari huyo wa zamu,alifanya juhudi na kufanikiwa kupata mshipa kichwani na kumwekea Sisilia dripu kichwani.Hata hivyo,  Juni, 8 mwaka huu,mtoto huyo aliweza kupewa rufaa kwenda hospitali ya St.Gasper ya Itigi, baada ya hali yake kubadilika na kuwa mbaya,” alisema Mamanda Magiligimba.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo alisema Juni, 15 mwaka huu saa tano asubuhi, mtoto Sesilia alifariki dunia wakati bado akiendelea kupata matibabu.
“Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa chanzo cha kifo hicho,ni tatizo la moyo. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wauguzi kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao,” alisema Magilingimba.
Habari kutoka kwa mwajiri wa wauguzi hao,ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manyoni, wauguzi hao tayari wameisha simamishwa kazi kutokana na uzembe huo..
 
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Charles Fussi, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kutokana na kukaa na uongozi wa hospitali hiyo na watuhumiwa kikuri kosa.
Na Nathaniel Limu, Singida

0 comments:

Post a Comment