MTOTO wa miaka nane alifariki jana Jumapili huko Bumula, katika Kaunti ya Bungoma nchini Kenya, wakati mama yake alipomwacha katika gari lililofungwa.
Mwanamke huyo na mpenzi wake wanasemekana walikwenda katika chumba cha nyumba ya wageni karibu na soko la Mateka na kumwacha mwanawe ndani ya gari likiwa limezimwa na kufungwa kabisa madirisha.
Mkuu wa Polisi wa Mateka Julius Barasa alisema mwanamke huyo alitambuliwa kama Christine Nasimivu.
“Walimwachia chupa tatu za soda lakini mtoto alifariki kutokana na kukosa hewa safi,” alisema afisa huyo wa polisi.
Polisi waliwaokoa wawili hao kutoka kwa wananchi wenye hasira ambao walikuwa wanataka kuwanyonga.
Wawili hao walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Bumula wakati mwili wa mtoto ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Bungoma.
Joseph Lupao, afisa mwangalizi wa watoto, aliwashutumu wawili hao kwa kumwacha mtoto peke yake ndani ya gari.
“Hii ni ajabu na jambo bay asana – mtoto amefariki kutokana na uzembe. Wanapaswa kushitakiwa mahakamani,” alisema.
Kulingana na tovuti ya Kidsandcars.com, watoto ambao huachwa ndani ya magari hufariki kutokana na joto la gari.
Tovuti hiyo inaeleza kwamba ndani ya gari joto huongezeka kwa haraka linapokuwa limefungwa, na linaweza kufika hata nyuzi joto 125 ndani ya dakika chache.
Joto hilo linasababisha joto la mwili wa mtoto kupanda na kufika zaidi ya nyuzi joto 40, na kusababisha kifo. Tovuti hiyo inasema kwamba mwili wa mtoto hupata joto kwa haraka mara tatu hadi tano zaidi ya ule wa mtu mzima.
0 comments:
Post a Comment