Thursday 15 June 2017

Idadi ya maambukizi ya virusi vya HIV kwa watoto wanaozaliwa yapungua takriban kwa asilimia 50 kati ya mwaka wa 2013 na 2015



Idadi ya maambukizi ya virusi vya HIV kwa watoto wanaozaliwa vimepungua takriban kwa asilimia 50 kati ya mwaka wa 2013 na 2015. Taarifa hizi za kutia moyo zilitangazwa na mama wa taifa Bi Margaret Kenyatta katika hafla ya kusheherekea ufanisi wa mpango wa Beyond Zero kwenye ukumbi wa Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

Ifikapo mwaka wa 2021, taifa la Kenya lina mipango na mikakati ya kumaliza maambukizi ya virusi vya HIV kwa watoto wanaozaliwa. Kwenye hafla ya kusheherekea ufanisi wa mpango wa Beyond Zero, mpango ulionzishwa na mkewe rais wa taifa la Kenya Bi Margaret Kenyatta, ilibainika idadi ya maambukizi ya virusi vya HIV imeshuka kwa kiasi kikubwa sana.

Mpango wa Beyond Zero ulianzishwa na Bi Kenyatta kuwasaidia akina mama wajawazito kujifungua salama salmini ili kuzuia maafa kwa watoto wakati mama mja mzito anapojifungua.

Takwimu mpya zinaonyesha kuwa mambukizi ya virusi vya UKIMWI yamepungua kwa asilimia 50 tangu mwaka wa 2015, kwa hisani ya mradi wa Beyond Zero.

Hiyo Jumanne, Bi Kenyatta alisema kuwa mwaka wa 2015, kati ya wanawake wajawazito 79,000 waliokuwa wakiishi na virusi vya UKIMWI, ni 6,600 pekee waliowaambukiza wanao wakati wa kujifungua. Idadi hii ilikuwa ndogo sana ikilinganishwa na ile ya mwaka wa 2013, ambapo maambukizi 12,000 ya mama kwa mtoto yalishuhudiwa.

'Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba kati ya wanawake 79,000 wenye virusi vya UKIMWI mwaka wa 2015, ni 6,600 pekee waliwaambukiza watoto wao wakati wa kujifungua. Maambukizi haya yalipunguwa kwa asilimi 50 kutoka 12,000 mwaka wa 2013. Takwimu zilizopo za mwaka wa 2016, tulikuwa na maambukizi chini ya 4,000 kote nchini. Mwaka uo huo wa 2016, wanawake wajawazito wapatao 59,400 kati ya 72,000 walipata msaada na mawaidha ya jinsi ya kujilinda na kuzuia kumwambukiza mtoto virusi vya UKIMWI kwa wajawazito walioathirika. Harakati hizi zilihakikisha kwamba tunatumia vyema rasilimali zilizopo .'

Vile vile, visa vya akina mama wajawazito kufariki wanapojifungua vilipungua kutoka 6,000 hadi 4,000 kwa mwaka. Bi Kenyatta alikuwa akizungumza kwenye ukumbi wa michezo wa Moi Kasarani, alipokuwa akizindua mradi wa kumaliza maambukizi ya virusi vya UKIMWI na magonjwa ya zinaa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto haswa kutoka mwaka 2016 hadi mwaka wa 2021. Bi kenyatta alipongeza serikali za kaunti kwa ushirikiano wao kwenye mafanikio ya Beyond Zero. Kufikia sasa ni zaidi ya wakenya laki nne wamefaidika na mradi huu.

Uzinduzi wa mpango huu ni habari njema kwa akina mama wajawazito wanaoishi na virusi vya UKIMWI na hata kwa wale wenye virusi na wangependa kupata watoto. Caroline Ngesa ni mama wa watoto watatu. Alijua ana virusi vya UKIMWI miaka kumi iliyopita, alipokuwa na uja uzito wa pili. Anasimulia jinsi mambo yalivyokuwa hapo awali…

'Na hiyo si kama sai unaongeleshwa. Ile ulikuwa unaambiwa uko positive, shika dawa enda umeze...hivyo..'

Mambo yalikuwa shwari alipopata mtoto wake wa tatu kwa sababu sasa alikuwa amepokea mafunzo ya jinsi ya kuzuia maambukizi kwa mtoto na vile vile uwepo wa dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI. Watoto wake wote watatu hawana virusi. Kwa sasa Caroline ni mshauri wa akina mama wajawazito wanaopitia wakati mgumu baada ya kubainika kuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI.

'Na ninaambia wamama wengine, once umeenda antenatal, ukapimwa na kupatikana una virusi, anza dawa mara moja. Kuwa na imani kwamba utazaa mtoto negative na utaishi maisha marefu..'

Mpango huu mpya ambao umeanzishwa na Bi Margaret Kenyatta utasaidia kuhakikisha kuwa kliniki zinaletwa karibu na akina mama wajawazito ili kuwafaa zaidi. 

0 comments:

Post a Comment