Saturday 17 June 2017

DKT. MABODI: CCM INAFANYA SIASA ZA USHINDANI WA SERA ZA MAENDELEO.


 ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Abdulla Juma Saadalla “ Mabodi” amesema CCM itaendelea kufanya ushindani wa sera za maendeleo zitakazowanufaisha wananchi wa makundi yote mijini na vijijini.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo ya Wanawake na Uongozi kwa wanachama na viongozi wa UWT Mkoa wa Mjini huko Amani Zanzibar, Dkt. Mabodi alisema wananchi wa visiwa vya Zanzibar kwa sasa wanachohitaji ni siasa za ushindani wa kisera katika kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja hadi taifa kwa ujumla.

Dkt. Mabodi alisema taifa lolote linalotamani kuendelea kiuchumi ni lazima wananchi wake wakubali kwa vitendo dhana ya siasa za ustaarabu katika kudumisha amani na utulivu wa nchi ili kufanya kazi za kujiongezea kipato na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo alisema ushindi wa CCM katika chaguzi mbali mbali za dola unatokana na nguvu za Wanawake wa UWT katika kuunga mkono harakati mbali mbali za kisiasa hadi kuhakikisha chama kinaingia madarakani.

“ kila mtu ndani ya Chama Chetu anajua na kutambua mchango wa Wanawake katika medali za kisiasa, wao ndio wamekuwa mstari wa mbele kwa kila kitu ikiwemo kujitokeza kwa wingi kupiga kura halali za kuiletea ushindi CCM.

Pia nakuahidini kwamba nitaendelea kuwa nanyi bega kwa bega kwa lengo la kuimarisha chama na jumuiza zake sambamba na kuwaletea wananchi maendeleo ya kudumu.”, alisema Dkt. Mabodi.

0 comments:

Post a Comment