Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria, sambamba na kutuma barua mbili za malalimiko yake kwa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo, limekosoa vikali operesheni za mauaji zinazofanywa na muungano unaoongozwa na Marekani nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, imeutaka Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo kutekeleza mjukumu yao ya kukomesha mauaji na uharibifu mkubwa unaofanywa na ndege za muungano bandia dhidi ya Daesh unaoongozwa na Marekani nchini Syria, sambamba na kulaani mauaji hayo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mashambulizi ya anga ya ndege za muungano huo, yamekuwa yakiwalenga tu raia wasio na hatia kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, vitendo ambavyo ni sawa kabisa na vile vinavyofanywa na magenge ya kigaidi ya Daesh (ISIS), Jab'hatu Nusra na mfano wa hayo huko Syria.
Jumatano ya jana, makumi ya raia wa Syria wakiwamo watoto waliuawa katika shambulio la anga la muungano wa kijeshi wa Marekani katika mkoa wa kaskazini wa Raqqah nchini Syria. Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema kuwa, jinai hizo zinazofanyika kwa makusudi kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, haziwezi kuvumilika.

Inafaa kuashiria kuwa, kwa mara kadhaa ndege za muungano huo, zimekuwa zikilenga kwa makusudi maeneo ya jeshi la Syria na raia wa kawaida kwa kisingizio hicho cha kupambana na ugaidi, suala ambalo limekuwa likilalamikiwa na serikali ya Damascus katika vyombo vya kimataifa. Aidha muungano huo unaendesha operesheni zake nchini Iraq na Syria bila ya kibali cha Umoja wa Mataifa au cha serikali za Baghdad na Damascus.
0 comments:
Post a Comment